Alhamisi, 14 Agosti 2014

UKAWA KUANDAMANA NCHI NZIMA KUMSHINIKIZA RAIS KUSITISHA BUNGE LA KATIBA



Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umemtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma na iwapo hatafanya hivyo utaongoza maandamano nchi nzima.
Umoja huo pia umeeleza kuwa kuendelea kwa Bunge hilo ni sawa na kuvuruga mchakato wa kupata Katiba Mpya, kuiweka nchi rehani, kufuja fedha za walipakodi, kuwahadaa Watanzania kwa kupitisha Katiba isiyotokana na maoni yao, huku kanuni zikibadilishwa na kuingizwa mambo ya Tanganyika katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kadhalika, umemtaka Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha za Bunge hilo kwa maelezo kuwa zinatumika bila maelezo sahihi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mwenyekiti mwenza wa umoja huo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) akiwa na wenyeviti wenzake, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), alisema hawatataja muda lakini wanataka jambo hilo lifanyike haraka iwezekanavyo.
“Iwapo Rais Kikwete hatatumia mamlaka yake kusitisha Bunge na kukubali liendelee kinyume na matakwa ya wananchi, Ukawa tutawaongoza Watanzania kupaza sauti kupinga najisi inayotiwa kwenye maoni yao, kupitia maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima,” alisema Mbatia.
Akizungumzia iwapo Rais anayo mamlaka ya kusitisha vikao vya Bunge hilo, Wakili na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jesse James alisema anaweza kufanya hivyo kwa kutumia dhamana ya uongozi aliyonayo, lakini kisheria hawezi kutokana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kutokuwa na ibara inayompa mamlaka hayo.
“Rais ni Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa nchi na Serikali. Majukumu hayo ndiyo yanayomfanya awe na uwezo wa kusitisha shughuli za Bunge hilo, hasa akiona theluthi mbili ya wajumbe kutoka kila upande kwa ajili ya kufanya uamuzi haitapatikana.”
Aprili 16, mwaka huu wajumbe wanaotokana na vyama vya siasa vinavyounda Ukawa na baadhi kutoka Kundi la 201, walisusia vikao vya Bunge hilo wakitaka msingi wa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba usibadilishwe, wakipinga uamuzi wa CCM kutaka kuingiza mfumo wa serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa katika rasimu.
Mbatia alisema Ukawa imechukua uamuzi wa kuandamana kutokana na wajumbe wa CCM pamoja na wengine 166 walioteuliwa kupitia kundi la wajumbe 201, kuendelea na vikao vya Bunge hilo na kuingiza mambo yao katika Rasimu ya Katiba, huku wakilipwa fedha za walipakodi.
“Mambo wanayoyajadili na kuyachomeka kinyemela kwenye rasimu kama ardhi, elimu, maji, kilimo, uvuvi, mifugo na serikali za mitaa ni masuala yanayopaswa kuandikwa kwa kina ndani ya Katiba ya Tanganyika siyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Zanzibar walijadili wenyewe mambo yao ya ndani na kutengeneza Katiba yao, hivyo hatuoni mantiki ya wajumbe kutoka Zanzibar kujadili na kuamua mambo ya Tanganyika. Bunge la Katiba halina sifa za kujadili mambo yasiyo ya muungano. Hii inaonyesha CCM wamelewa madaraka.”
Alisema ili Bunge hilo lipate uhalali wa kuendelea yanatakiwa kufanyika maridhiano ya pande zote zinazovutana na kusisitiza kuwa kinachoendelea sasa kinatokana na kukosekana kwa uongozi wa kisiasa.Source:Mwananchi

0 comments:

Chapisha Maoni