Alhamisi, 14 Agosti 2014

Miss Ethiopia ndiye Miss Africa Usa 2014, Joy Kalemera awa wanne.


Miss Ethiopia akifurahia taji la kuwa Miss Africa katika mashindano hayo yaliyofanyika Rockville, Maryland nchini Marekani na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Balozi wa Tanzania nchini Marekani. Mshiriki wa Tanzania, Joy Kalemera ameshika nafasi ya 4 kati ya washiriki 20 walioingia fainali hizo.
IMG_2395
Washiriki watano waliopata nafasi ya kuingia tano bora kutoka kushoto ni Miss Tanzania aliyeshika na 4, Miss Uganda aliyeshika na 2, Miss Ethiopia aliyeshinda, Miss Guinea aliyeshika namba 3 na Miss Nigeria aliyeshika namba 5.

Washindi namba 2 mpaka 4 wakiangalia Miss Ethiopia akivishwa taji, kushoto ni miss Cameoon aliyekua Miss Africa USA msimu uliopita.
Washiriki wote 20 katika picha ya pamoja.
Miss Ethiopia akipata picha ya pamoja na washindi namba 2 na 3 ambaye ni Miss Uganda na Miss Guinea.
Miss Ethiopia katika picha ya pamoja na mshindi namba 2 Miss Uganda.

ELIZABETH TARIMO NDIYE MSHINDI WA TAJI LA MISS KANDA YA MASHARIKI 2014


Mshindi wa Taji la Redd’s Miss Kanda ya Mashariki 2014 ,  Elizabeth  Tarimo (18) ambaye pia ni Miss Lindi akiwa mwenye uso wa furaha na tabasamu la ushindi sambamba na  mshindi wa pili  Nidah Katunzi (19) ( kulia) ,ambaye ni Miss Mtwara pamoja na wa tatu, Lucy Julius Diyu  (21) (kushoto) Miss Morogoro baada ya kutangazwa kuwa washindi kwenye nafasi hizo wakati  kinya’ganyiro cha kuwania taji hilo  kilichofanyika juzi usiku kwenye ukumbi wa Hoteli ya Nashera ya mjini Morogoro.

UKAWA KUANDAMANA NCHI NZIMA KUMSHINIKIZA RAIS KUSITISHA BUNGE LA KATIBA



Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umemtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma na iwapo hatafanya hivyo utaongoza maandamano nchi nzima.
Umoja huo pia umeeleza kuwa kuendelea kwa Bunge hilo ni sawa na kuvuruga mchakato wa kupata Katiba Mpya, kuiweka nchi rehani, kufuja fedha za walipakodi, kuwahadaa Watanzania kwa kupitisha Katiba isiyotokana na maoni yao, huku kanuni zikibadilishwa na kuingizwa mambo ya Tanganyika katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kadhalika, umemtaka Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha za Bunge hilo kwa maelezo kuwa zinatumika bila maelezo sahihi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mwenyekiti mwenza wa umoja huo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) akiwa na wenyeviti wenzake, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), alisema hawatataja muda lakini wanataka jambo hilo lifanyike haraka iwezekanavyo.
“Iwapo Rais Kikwete hatatumia mamlaka yake kusitisha Bunge na kukubali liendelee kinyume na matakwa ya wananchi, Ukawa tutawaongoza Watanzania kupaza sauti kupinga najisi inayotiwa kwenye maoni yao, kupitia maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima,” alisema Mbatia.
Akizungumzia iwapo Rais anayo mamlaka ya kusitisha vikao vya Bunge hilo, Wakili na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jesse James alisema anaweza kufanya hivyo kwa kutumia dhamana ya uongozi aliyonayo, lakini kisheria hawezi kutokana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kutokuwa na ibara inayompa mamlaka hayo.
“Rais ni Amiri Jeshi Mkuu, Mkuu wa nchi na Serikali. Majukumu hayo ndiyo yanayomfanya awe na uwezo wa kusitisha shughuli za Bunge hilo, hasa akiona theluthi mbili ya wajumbe kutoka kila upande kwa ajili ya kufanya uamuzi haitapatikana.”
Aprili 16, mwaka huu wajumbe wanaotokana na vyama vya siasa vinavyounda Ukawa na baadhi kutoka Kundi la 201, walisusia vikao vya Bunge hilo wakitaka msingi wa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba usibadilishwe, wakipinga uamuzi wa CCM kutaka kuingiza mfumo wa serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa katika rasimu.
Mbatia alisema Ukawa imechukua uamuzi wa kuandamana kutokana na wajumbe wa CCM pamoja na wengine 166 walioteuliwa kupitia kundi la wajumbe 201, kuendelea na vikao vya Bunge hilo na kuingiza mambo yao katika Rasimu ya Katiba, huku wakilipwa fedha za walipakodi.
“Mambo wanayoyajadili na kuyachomeka kinyemela kwenye rasimu kama ardhi, elimu, maji, kilimo, uvuvi, mifugo na serikali za mitaa ni masuala yanayopaswa kuandikwa kwa kina ndani ya Katiba ya Tanganyika siyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Zanzibar walijadili wenyewe mambo yao ya ndani na kutengeneza Katiba yao, hivyo hatuoni mantiki ya wajumbe kutoka Zanzibar kujadili na kuamua mambo ya Tanganyika. Bunge la Katiba halina sifa za kujadili mambo yasiyo ya muungano. Hii inaonyesha CCM wamelewa madaraka.”
Alisema ili Bunge hilo lipate uhalali wa kuendelea yanatakiwa kufanyika maridhiano ya pande zote zinazovutana na kusisitiza kuwa kinachoendelea sasa kinatokana na kukosekana kwa uongozi wa kisiasa.Source:Mwananchi

JK AFANYA UTEUZI WA MAJAJI WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA WAPYA 20.








Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, baada ya kushauriana na Tume ya Utumishi wa Mahakama, amewateua wafuatao kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuanzia tarehe 13 Agosti, 2014.
WATUMISHI WA MAHAKAMA
(i)                 Bw. Penterine Muliisa KENTE, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani, Dar es Salaam.
(ii)               Bw. Benedict Bartholomew MWINGWA, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Msajili wa Mahakama Kuu, Dar es Salaam.
(iii)             Bw. Edson James MKASIMONGWA, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Katibu wa Jaji Mkuu.
(iv)             Bw. David Eliad MRANGO, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Msajili, Baraza la Ushindani, Dar es Salaam.
(v)               Bw. Mohamed Rashid GWAE, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Msajili, Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi, Dar es Salaam.
(vi)             Dkt. John Eudes RUHANGISA, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Msajili, Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Arusha.
(vii)           Bw. Firmin Nyanda MATOGORO, ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Naibu Mwenyekiti, Baraza la Rufaa la Kodi, Dar es Salaam.
MAWAKILI WA SERIKALI NA TAASISI MBALIMBALI ZA SERIKALI
(i)                 Dkt. Eliezer Mbuki FELESHI, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Mkurugenzi wa Mashitaka, Dar es Salaam.
(ii)               Bi. Barke Mbaraka Aboud SEHEL, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Kaimu Mkurugenzi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dar es Salaam.
(iii)             Bi. Winfrida Beatrice KOROSSO ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Katibu Mtendaji, Tume ya Kurekebisha Sheria, Dar es Salaam.
(iv)             Bi. Lilian Leonard MASHAKA, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,                      (TAKUKURU), Dar es Salaam.
(v)               Bi. Leila Edith MGONYA, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Msaidizi wa Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dar es Salaam.
(vi)             Bw. Awadhi MOHAMED, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Mchunguzi Mkuu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKURURU), Dar es Salaam.
MAWAKILI WA KUJITEGEMEA
(i)                 Bw. Lugano J.S. MWANDAMBO, kutoka REX Attorneys, Dar es Salaam.
(ii)               Bw. Amour Said KHAMIS, kutoka AKSA Attorneys, Dar es Salaam.
(iii)             Dkt. Paul KIHWELU, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Wakili wa Kujitegemeana na Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu Huria, Dar es Salaam.
(iv)             Bi. Rose Ally EBRAHIMU, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Wakili wa Kujitegemea, Bulyankulu Gold Mine Ltd, Shinyanga.
(v)               Bi. Salma MAGHIMBI, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Mjumbe, Tume ya Ushindani, (FCC), Dar es Salaam.
WATUMISHI WA VYUO VIKUU
(i)                 Dkt. Mary Caroline LEVIRA, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Kaimu Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha.
(ii)               Dkt. Modesta Opiyo MAKOPOLO, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu, Mzumbe, Morogoro.
Wateuliwa wote wataapisha tarehe 15 Agosti, 2014 Saa 05.00 asubuhi katika Viwanja vya Ikulu Dar es Salaam.
Imetolewa na Mkurugenzi Idara ya habari Maelezo13 Agosti, 2014