Wakati
wabunge wakiijia juu Wizara ya Elimu na Mafunzo kutokana na kuwepo kwa
hali ya kuporomoka kwa kiwango cha elimu nchini, kashfa ya aina yake
imeibuka ikihusisha wizara hiyo kumtumia Makamu wa Rais Dk. Gharib Bilal
kuwapa zawadi hewa wanafunzi 10 bora wa mwaka jana.
Taarifa
zilizozifikia NIPASHE zinasema tukio hilo ilifanyika Mei 10 wakati wa
kilele cha Wiki ya Elimu nchini iliyofanyika mkoani Dodoma, ambapo Dk.
Bilal alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hizo.
Imefahamika
kwamba viongozi wa wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri
Mkuu, Wizara ya Tawala ya Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
walimpatia Dk. Bilal bahasha tupu ambazo aliwapa wanafunzi hao kwa
maelezo ndani yake kulikuwa na kiasi cha Sh. 250,000 kila moja.
Katika
bahasha hizo za rangi tofauti moja ikiwa ya rangi ya khaki na nyingine
nyeupe iliyofifia yenye nembo ya serikali, zilitolewa kwa wanafunzi kumi
wa shule za sekondari waliofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha
nne mwaka 2013.
Katika
mchanganuo huo, wanafunzi hao walitakiwa kupewa Sh. 500,000 kama zawadi
kutoka serikalini, Sh. 250,000 kutoka Ubalozi wa China na Sh. 500,000
ya vocha ya kununua vitabu vya kiada na ziada.
Katika
hali ya kushangaza, wakati wanafunzi hao walipoitwa jukwaani
kukabidhiwa zawadi zao, waligundua ndani hakukuwa na kitu na kusababisha
kuibuka kwa malalamiko kutoka kwa wazazi walioambatana nao.
HALI HALISI DODOMA
Baadhi
ya wazazi wakiongea na NIPASHE walisema shughuli nzima ya utoaji tuzo
haikuwa na mpangilio mzuri kitu ambacho kilisababisha wazazi na watoto
wao kupata tabu walipokuwa mjini Dodoma.
Mmoja
wa wazazi hao Caroline Marealle ambaye mtoto wake Joyceline Leonard
(17), alikuwa mmoja wa wanafunzi waliozawadiwa, alisema dalili mbaya
walianza kuiona mara baada ya kufika Dodoma siku moja kabla ya sherehe
baada ya kutelekezwa na wizara hiyo ndani ya jengo la Sekondari ya
Dodoma.
Alisema
walijaribu kuwasiliana na mratibu wa elimu kutoka wizarani kwa ajili ya
kupata maelekezo ya mahali watakapofikia na chakula, lakini
alipotafutwa hakuwa na jibu la kutoa na kisha aliamua kuzima simu yake
ya mkononi.
“Tulibaki
tukihangaika pale shuleni hatujui wapi tuelekee, baada ya kukaa sana
tuliamua tuwachukue watoto wetu tukaenda kutafuta sehemu ya kujistiri,”
alisema Marialle.
UTATA WAIBUKA UWANJANI
Siku ya pili yake ya Mei 10, wazazi na watoto wao walijumuika katika Uwanja wa Jamhuri ambako sherehe hiyo ilifanyika.
Uwanjani
hapo pamoja na kuwepo kwa Makamu wa Rais, pia viongozi mbalimbali
walihudhuria akiwamo Waziri wa Elimu na Mafunzo, Shukuru Kawambwa,
Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia, wakuu wa mikoa, wilaya, wabunge na
viongozi mbalimbali.
Katika
taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Elimu nchini, Prof. Eustella
Bhalalusesa iliyosomwa mbele ya Makamu wa Rais, ilionyesha zawadi
zitakazotolewa ni halisi na kwamba imelenga kutekeleza kikamilifu mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Katika
taarifa hiyo ilieleza kwamba zawadi hizo za Sh. 250,000 zingekwenda kwa
washindi 10 wa sekondari na Sh. 150,000 kwa washindi wa shule ya
msingi.
Aidha, China ilitoa Sh. milioni 25 ambapo kwa wanafunzi 100 waliofanya vizuri wangepata Sh. 250,000 kila mmoja.
Aidha, Sh. 500,000 zilitolewa kama vocha ya vitabu na Mfuko wa Elimu nchini (TEA).
Mkanganyiko
ulianza wakati wa kuitwa kwa majina ya wanafunzi bora wa sekondari,
ambapo katika majina hayo mawili ya wanafunzi wa kike yalikatwa na
nafasi zao zilijazwa na wanafunzi wa kiume walioshika nafasi ya 11 na 12
kitaifa.
Majina ya wanafunzi waliokatwa ambao pia walifika uwanjani kupata zawadi ni Janeth Urassa na Angel Ngulumba.
“Tuliambiwa
majina yao yaliondolewa ili kupisha nafasi kwa wanafunzi wa kiume, kitu
hicho kilisababisha simanzi kwa wazazi wa wanafunzi hao ambao walifika
hapo kuona watoto wao wakipewa zawadi lakini ilishindikana,” alisema
mzazi mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe
gazetini.
Wanafunzi
waliotajwa na kutakiwa kufika mbele ya Makamu wa Rais ni Robina
Nicholaus wa Shule ya Marian Girls, Magrath Kakoko (St Francis),
Joyceline Marealle (Canossa), Safarina Mariki na Abby Sembuche (Marian
Girls).
Wengine
ni Sunday Mrutu kutoka (Anne Marie), Nelson Rugola Anthony na Emmanuel
Mihuba Gregory (Kaizirege-Kagera), huku waliongezwa ni Razack Hassan (St
Matthew’s) na Hamis Msangi (Eangles).
Utata
zaidi ulendelea kuibuka pale ilipofika kipindi cha utoaji zawadi,
ambapo kila mwanafunzi aliyeshuka kutoka jukwaani alionekana kushtuka
baada ya kugundua bahasha zao hazikuwa na kitu ndani.
Kipindi hicho matangazo yalisikika uwanjani hapo kwamba kwenye bahasha kulikuwa na kiasi hicho kama kuwapa mkono wa hongera.
“Tulianza
kuwa na wasiwasi na jambo hilo, tulianza kuhangaika kumtafuta mratibu
atupe ufafanuzi zawadi za watoto zilikuwa wapi kwani tayari tuligundua
wenzetu sio wakweli,” alisema mzazi mwingine.
Baada
ya kugundua jambo hilo walijaribu kuwatafuta wahusika, walipofanikiwa
kuwapata waliwaambia jambo hilo lilifanyika kwa bahati mbaya hivyo
waliahidi kulirekebisha haraka kwa kuwapa stahiki zao.
ZAWADI ZATOLEWA KINYEMELA
Kutokana
na hali hiyo, wazazi waliokuwepo uwanjani hapo walianza kulalamika na
kuwafuata viongozi wa wizara hiyo ili kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo.
Hata hivyo, viongozi hao waliwataka wasubiri hadi mwisho wa sherehe ndipo watapewa pesa hizo.
Taarifa
hizo zinasema katika kusubiria zawadi hizo ilibidi kukaa uwanjani kwa
saa sita kuanzia majira ya saa 7:00 mchana wakati sherehe hizo
zilipomalizika.
Lingine
la kushangaza hata katika chakula kilichoandaliwa katika chuo cha Mt.
Gasper, wanafunzi hao na wazazi hawakwenda badala yake waliachwa
uwanjani wakiungua jua hadi jioni.
“Hakuna
mtu aliyekumbuka kama wanafunzi waliachwa pale uwanjani, tulikaa pale
bila kupata chakula wala maji hakuna aliyestuka,” alilalamika Marialle.
Ilipofika
muda wa saa 12:00 jioni maafisa kutoka wizarani walifika na kuanza
kutoa pesa walizodai zimetoka serikalini pamoja na sh. Sh. 90,000 kwa
kila mtu kama za kujikimu. Hata hivyo, pesa zingine zile za vocha na
Ubalozi wa China hawakupatiwa kwa maelezo bado hatua muhimu
hazijafikiwa.
PESA ZA CHINA ZAYEYUKA
Sh. Milioni 40 zilizotolewa na China wa ajili ya kuwazawadia wanafunzi hao hazijulikani lini zitatolewa.
Uchunguzi
wa gazeti hili umebaini pesa hizo zimetolewa kupitia Tamisemi na
ilipaswa kutolewa kwa wanafunzi 100 kwa shule za sekondari na msingi
zilizofanya vizuri nchini. Hata hivyo, kumekuwa na hali ya ukimya kutoka
Wizara hiyo kuzungumzia namna ya utoaji wa pesa hizo kwa wahusika.
Alipotafutwa
Naibu waziri wa Tamisemi anayeshughulikia Elimu, Kassim Majaliwa,
kupitia simu yake ya mkononi, hakupatikana baada ya msaidizi wake
aliyepokea simu kujibu Waziri huyo yupo kwenye kikao cha uchangiaji
madawati mkoani Lindi.
WIZARA YAPATA KIGUGUMIZI
Alipotafutwa
Kamishna wa Elimu Prof. Bhalalusesa kuzungumzia jambo hilo hakuwa
tayari kuzungumzia kwa kile alichosema yupo kwenye kikao muhimu.
“Nakuomba
ndugu mwandishi siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa kwani nipo
kwenye kikao muhimu naomba unielewe tafadhali,” alisema.
TEA WAOMBA RADHI
Uongozi
wa Mfuko wa Elimu (TEA) umeomba radhi kwa wazazi na wanafunzi kwa hali
mbaya iliyojitokeza walipokuwa Dodoma, ambapo walisema jambo hilo
halitajirudia tena.
Akizungumza
na gazeti hili, Afisa Habari wa mfuko huo, Sylvia Gunze, alisema
wamesikitishwa na mkanganyiko uliojitokeza na kueleza kwamba pesa
zilizotolewa za vocha zingetolewa kuanzia jana.
“Kupewa
vocha sio jambo geni kwa wanafunzi waliofanya vizuri, wizara husika
ilikuwa ikifanya hivyo kila mwaka lakini mwaka huu kulikuwa na
mkanganyiko kidogo hata hivyo, hali imetengemaa na wahusika wanaanza
kulipwa,” alisema Gumze.
Alisema
kwenye bahasha walizopatiwa walifanya kosa la kutotoa ufafanuzi kuwa
ndani yake kulikuwa na karatasi iliyoandikwa namba za simu ambazo wazazi
wangezitumia kwa ajili ya kuwasiliana ili kupata pesa hizo.