UNAPOTAKA
kutaja majina ya vijana chipukizi, ambao sasa wanaogelea katika bahari
ya ustaa , basi huwezi kuliweka mbali jina la Ommy Dimpoz , mkali wa
vibao vikali vya Baadaye na Tupogo. Hizi ngoma mbili zimekimbiza sana na
nadhani ndizo zinazompa shoo nyingi , ndani na nje ya nchi , ingawa pia
hivi karibuni aliingiza mtaani kazi yake nyingine inayokwenda kwa jina
la Ndagushima.
Katika vitu huwa napenda , basi ni
kujaribu kuwa mkweli kwa kadiri ninavyoweza. Mimi ni shabiki mkubwa wa
nyimbo hizi mbili, ninazipenda sana kuzisikiliza ingawa sidhani kama
zina ujumbe wa viwango hivyo .
Ni kazi za kiburudani zaidi , hasa
unapokuwa umetoka kwenye kazi ngumu ya kufikirisha ubongo kama hizi
zetu. Staili yake ya muziki imemfanya kuwa kipenzi kikubwa kwa mashabiki
na ukichanganya na ubitozi wake , basi siyo jambo la ajabu kuona kwamba
kwa muda mfupi tu tangu amepata jina kimuziki, amepata shoo nyingi nje
ya nchi , kiasi cha kumfanya awe miongoni mwa mastaa wanaoingiza mkwanja
wa kutosha , kama shoo za nje zinaweza kuwa kigezo cha kupata zaidi .
Sijawahi kukaa na huyu bwana mdogo hata siku moja katika ile hali ya
kubadilishana mawazo, hivyo sitatenda haki kama nitajaribu kumhukumu kwa
mambo ambayo sina uhakika nayo , ingawa baadhi ya matendo mbele ya watu
yanaweza kusaidia kutafsiri tabia ya mtu!
Jumapili
iliyopita, Juni 1, 2014 dogo alikuwa miongoni mwa wasanii waliohudhuria
shoo kubwa ya uzinduzi wa kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam
uliofanyika katika Viwanja vya Mwembeyanga. Wasanii wengi walikuwepo na
walifanya vizuri kwa kweli . Tatizo langu lilikuwa moja tu , kwa huyu
chipukizi ambaye kama ataendelea kukaza buti kama hivi , basi haina
shaka kwamba anaweza kuwa mojawapo ya alama za muziki wa kizazi kipya
katika ulimwengu wa burudani . Wakati akipanda jukwaani , mashabiki kwa
mamia , hawakuwa wamechangamka kama alivyotegemea na ili kuwaamsha,
alivua kofia yake na kuwatupia .
Baada ya hapo akawatupia pia
miwani. Hivi ni vitu vya kawaida kufanywa na mastaa wakubwa, inawafanya
mashabiki kutambua jinsi gani mtu wao anavyowathamini . Na siyo wasanii
wa muziki tu ambao hufanya hivi , wanasoka , wacheza tenisi, mabondia,
madereva wa magari, wanariadha na wanamichezo wengine , huwarushia jezi ,
kofia na vitu vidogovidogo mashabiki wao . Ommy Dimpoz alifanya zaidi .
Baada ya kutupa vitu hivyo na kukuta mashabiki wakiwa bado hawajapanda
mzuka, alitoa shilingi elfu hamsini na kuwarushia.
Pata picha ya
patashika iliyotokea kwa mashabiki. Unajua alichokisema ? “Sisi wasanii
tunapata fedha nyingi kutoka kwenu nyinyi mashabiki wetu, kuonyesha
kuwajali , naomba niwarudishie.” Hiyo tisa , kumi, Dimpoz alizama tena ‘
chimbo ’ na kuibuka na kiasi cha kama laki mbili hivi na kuwarushia
tena watu waliojazana mbele yake ! Dah, sawa , wasanii wanapaswa
kurudisha sehemu ya mapato yao kwa jamii, lakini sidhani kama ni kwa
staili hii . Binafsi naona kama huu ni ushamba fulani hivi ! Mtu smati
kichwani hawezi kutupa hela kwenye umati wa watu , tena wa uswahilini
kama wa kule Temeke , unataka nini?
Naamini kabisa akitokea mtu
hata kwenye kumbi ambazo tunajua zina watu wa afadhali , wenye uwezo wa
kutoa kiingilio cha shilingi laki moja kama pale Mlimani City, bado
akiibuka ‘ mtu wa mawe ’ na kurusha mahela itakuwa mshikemshike ,
sembuse Mwembeyanga? Zipo namna za kurudisha hela kwa jamii yako , siyo
kwa wasanii tu , bali hata wafanyabiashara, kama wanavyofanya baadhi yao
kama Dr . Reginald Mengi na Mzee Mustafa Sabodo.
Tafuta sehemu
yenye shida ya maji , chimba kisima , angalia wenye shida ya huduma za
afya, jenga zahanati au nenda katika vituo vya watoto yatima wape nguo ,
madaftari au hata kula nao chakula . Jamii yetu ina maskini wengi ,
kuwatupia hela kama vile huwasaidii , bali utawaumiza kwa sababu
wataishia kugombana, kutoana ngeu na mwisho wa siku hakuna atakayeondoka
na pesa kwa sababu zote zitachanika katika purukushani . Naamini kwa
nilichokisema , Dimpoz atakuwa amenielewa. Source: Globe