Ukuaji wa deni la taifa waumiza vichwa wabunge.....Mpaka sasa kila mtanzania anadaiwa Tsh.600,000
Bunge la bajeti linaendelea bungeni mjini Dodoma ambapo sasa ni zamu ya wizara ya fedha na uchumi. Bajeti yake imewasilishwa na waziri wa fedha Saada Mkuya Salum ambapo bajeti yake imepita huku suala la deni la taifa likiendelea kuumiza vichwa vya wabunge wengi kwa kuendelea kukua siku hadi siku.
Suala hilo limeonekana kuwashtua wabunge wengi akiwemo Mheshimiwa
Christina Lissu ambaye anasema fedha zinazokopwa na kuongeza deni la
taifa zimekuwa hazitumiki katika miradi ya maendeleo.
Mhe. Lissu anasema “Mheshimiwa spika, tumeangalia
hotuba ya kamati ya wizara hii ikieleza kwamba deni la taifa limekua
kutoka trilioni 21 hadi 29 ikiwa ni ongezeko la trilioni 8 tu kwa miaka
7, kukopa ni sahihi na nchi yoyote inakopa lakini je fedha tunazokopa
zinaenda katika miradi ya maendeleo? Mbona ukuaji huu wa deni hauendani
na fedha zinazoelekezwa katika miradi ya maendeleo?.”
“Kwa mwaka huu karibu miradi yote ya maendeleo imepelekewa fedha
chini ya asilimia 50, mbona ukuaji wa deni hauendani na fedha zilizoenda
kwenye matumizi ya maendeleo? inawezekana tunakopa na tuaambiwa deni ni
stahimilivu lakini kama fedha haiendi kupunguza matatizo ya wananchi
inakuwa haina maana kukopa.”
Suala la kuchelewesha fedha zinazotengwa kwa ajili ya bajeti ya
miradi mbalimbali limeonekana kuwagusa wabunge wengi ambapo Mhe. Asupta
Mshana anasema;
“Kumekuwepo na tatizo kubwa la fedha tunazoidhinisha kama bunge
kutotolewa kwa wakati na kufanya kazi kama zilivyopangiwa, tatizo ni
kwamba tunaandaa bajeti kwa kutabiri bila kuwa na fedha mkononi. Ni
vyema tukabadilisha utaratibu wa kuandaa bajeti zetu badala ya kuwa na
Cash bajeti tuwe na Capital bajeti”
Pamoja na jitihada za serikali kupitia kukusanya kodi je mikakati ya ukusanyaji kodi inatosha? Mhe. David Kafulila anasema;
“Tufike mahala tuwe na mkakati wa kutosha kuhakikisha maeneo yote
ambayo hatukusanyi kodi tunakusanya. Tumezungumza mara kadhaa juu ya
watanzania kuashiriki kwenye uchumi wa nchi yao kwa kupitia masoko ya
mitaji katika soko la hisa DSE ili watanzania washiriki kwenye uchumi
wao, tusiwanyime fursa wazawa kushiriki katika uchumi wao.”
Wakati Serikali ikiendelea kubanwa juu ya suala hilo, Waziri Kivuli
wa Fedha, James Mbatia amesema ukiligawanya deni hilo kwa idadi ya
Watanzania milioni 45, kila mwananchi atakuwa anadaiwa Sh600,000.
0 comments:
Chapisha Maoni