Alhamisi, 8 Mei 2014

SABABU ZA BAADHI YA WANANDOA KULAZIMIKA KUCHEPUKA!


Kiukweli kabisa mchepuko siyo dili kwa kuwa wengi waliochepuka wamejikuta kwenye matatizo makubwa sana. Ndiyo maana tunashauriwa kubaki njia kuu kwa kujenga uaminifu kwa wale tuliotokea kuwapenda na kutodiriki kuwasaliti.

Lakini wakati ukweli ukiwa hivyo, kasi ya kusalitiana kwa wapenzi imekuwa ikiongezeka kila kukicha. Utulivu umekuwa sifuri, unayedhani katulia kesho utasikia kafumaniwa.
Unaweza kuwa na mpenzi ambaye kila mara anakueleza kuwa, hawezi kukusaliti na atakuwa na wewe katika shida na raha lakini huyohuyo usishangae siku moja ukamkuta yuko na mtu mwingine.
Swali la kujiuliza ni kwamba, kwa nini wapenzi wanashindwa kujizuia na mchepuko? Hivi hawaoni hatari iliyopo mbele yao kwa kuwasaliti wenza wao? Mimi nadhani kuna tatizo lakini hebu tuone sababu  ambazo zinaonekana kuwasukuma baadhi ya wanandoa kushindwa kutulia kwenye njia kuu.
Katika utafiti niliofanya nimebaini kuwa, tamaa za kijinga zimekuwa zikisababisha wengi kuwasaliti wenza wao na kuwasababishia maumivu makubwa sana.
Tamaa hasa ya pesa imekuwa ikiwashawishi baadhi ya watu kushindwa kujizuilia kusaliti. Kwa wale ambao wako kwenye ndoa wakati mwingine hasa wanawake wasipopatiwa mahitaji yao muhimu na akatokea jamaa, akamhakikishia kupata kila anachotaka, anakubali bila kujua kwamba anakosea.
Wengine wanapatiwa kila kitu na waume zao lakini sasa kinachotokea ni tamaa za kimwili tu ambazo zinawasumbua na kujikuta wanatafuta wanaume wengine huku wakidai kuwa wanatafuta ladha tofauti.
Lakini wengi wamekuwa wakichepuka kutokana na mazingira wanayojengewa na wenza wao.
Kwa mfano, unaweza kukuta mke anamuwekea mumewe vikwazo katika tendo la ndoa. Anampangia ratiba na wakati mwingine anapoombwa tendo anadai amechoka au anaumwa na sababu nyinginezo.
 Hivi katika mazingira kama haya unatarajia nini kutokana kwa mume kama siyo kuchepuka?
Kweli mume anaweza kuvumilia kwa kipindi fulani lakini ikafika wakati uvumilivu ukamshinda akaamua kutafuta mtu wa pembeni wa kumpa furaha.
Ndiyo maana wanaowanyima unyumba waume zao kwa kutoa visingizio mbalimbali hata wanaposikia kwamba wanasalitiwa, wanakuwa hawana nguvu ya kuwashutumu wapenzi wao, wataanzia wapi wakati hawawatimizii mambo flani?
Si hivyo tu, kwa wanaume nao wengine wamekuwa wakiwasusa wake zao na kukaa siku mbili ama zaidi bila kuonekana nyumbani na kama atarudi basi usiku akiwa amelewa na hana mpango kabisa na mke wake.
Katika mazingira hayo unadhani nini kinaweza kutokea kama siyo mwanamke kutafuta mwanaume atakayempatia mapenzi? Ni kweli kuchepuka ni hatari lakini mwanamke huyu naye ana hisia, kuna wakati anatamani kabisa kuwa na mtu wake faragha lakini inashindikana, hivi akitokea wa kumburudisha atakataa?
Sisemi kwamba, katika mazingira hayo suluhisho ni kusaliti lakini utafiti unaonesha kuwa, wapo wanawake ambao wamekuwa wakitoka nje ya ndoa zao kwa kutothaminiwa na wenza wao, matokeo yake wanajikuta wametoka nje ya njia kuu.
Lingine ambalo linaonekana kuwafanya wanandoa wengi kuchepuka ni kuwepo kwa mapenzi ya kilaghai. Tunapozungumzia mapenzi, tunaweza kuyagawanya katika makundi mawili, mapenzi ya kweli na mapenzi ya uongo. Walio katika mapenzi ya kweli huwezi kuwasikia wamesalitiana.
Ila wale walio katika mapenzi ya kudanganyana kusalitiana itakuwa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku. Hii ina maana kwamba, kama Amina hana mapenzi ya dhati kwa Juma basi ni rahisi sana Amina kufanya mapenzi na Ally ama John kwa siri.
Kwa maelezo hayo unaweza kuona ni kwa jinsi gani kutokuwepo na mapenzi ya dhati baina ya wawili waliokubaliana kuwa kitu kimoja kunasababisha kuwepo kwa mazingira mazuri ya kusalitiana.
Kwa kumalizia niseme tu kwamba, kusalitiana kwa wanandoa kumekuwa kukitokea kutokana na kuwepo kwa mazingira fulani ambayo baadhi yao wamekuwa wakishindwa kujizui nayo na hivyo kujikuta wanatoka nje ya mahusiano.
Ila sasa nalazimika kwa nguvu zote kuwashauri wale walio katika uhusiano wa kimapenzi, namaanisha wapenzi wa kawaida, wachumba ama wanandoa, kutokuwa na tamaa za kijinga na kufikia hatua ya kuwasaliti wapenzi wao.
Hivi unajisikiaje unapomvulia nguo mtu ambaye wala hana ‘future’ na wewe? Hivi na wewe ukifanyiwa hivyo na mpenzi wako utajisikiaje? Elewa maumivu utakayoyapata pale utakaposikia mpenzi wako ana uhusiano na fulani ni hayo hayo atakayoyasikia mwenza wako.
Kuwa muaminifu, ridhika na unachokipata kwake, muoneshe mapenzi ya dhati naye atafanya hivyo hivyo na kujikuta mnayafurahia maisha yenu.

0 comments:

Chapisha Maoni