Alhamisi, 8 Mei 2014

WANACHAMA SIMBA SC MSIDANGANYIKE NA SIASA NYEPESI ZA WACHUMIA MATUMBO


486618_545707472135474_901587883_n
TAYARI mchakato wa uchaguzi katika klabu ya Simba sc umeshaanza na tayari mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Damas Ndumbaro ametangaza kuwa juni 29 mwaka huu uchaguzi utafanyika
Wapo watu wengi wanaotamani kuiongoza klabu ya Simba ambayo kwasasa ipo katika hali ngumu kwa soka la uwanjani.
Kumaliza nafasi ya nne nyuma ya Mbeya City, Yanga na Azam fc ni jambo linalowaumiza wana Simba wote.
Ni msimu wa pili mfufulizo Simba wanakosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa. Kwa ukongwe wake ni jambo la fedheha kubwa japokuwa mpira uko hivyo.
Hatuwezi kuwakosoa Simba kwa matokeo waliyokuwa wanapata kwasababu mpira wa miguu huwa unabadilika, lakini makosa yanapotokea kwasababu ya watu fulani kutowajibika, hapo lazima ukosoaji uhusike.
Kwa mfano wachezaji kushindwa kucheza vizuri kwasababu hawajalipwa posho na mishahara, unashindwaje kuukosoa uongozi kwa kushindwa kuwajibika?
Kumekuwapo na mivutano ya muda mrefu baina ya mwenyekiti wa Simba, sasa Rais, Ismail Aden Rage na baadhi ya wajumbe wake wa kamati ya utendaji pamoja na baadhi ya wanachama.
Sinema nyingi zimeonekana na zimeandikwa, kila mtu anafahamu yaliyokuwa yanatokea Simba sc.
Jana aliyekuwa kiungo wa Simba sc msimu uliopita, Henry Joseph Shindika wakati akihojiana na mtandao huu alikiri wazi kuwa maisha ya wachezaji wa kitanzania ni magumu sana.
Joseph alisema watanzania tunajijua maisha yetu wenyewe. Kama si baba, basi ni kaka au ndugu, kwahiyo unapokuwa unapata kipato kuna watu wengi nyuma yako wanaohitaji msaada.
Kwahiyo utakuta mchezaji ana familia, anasomesha wadogo zake na anategemewa na wazazi wake kutokana na mshahara anaopata katika klabu.
Inapotokea hapewi mshahara mambo mengi yanakwama, hivyo kisaikolojia anaathirika na kushindwa kucheza vizuri na ndio maana unaona wachezaji hawana morali.
Maneno ya Joseph yana pointi kubwa ndani yake kuwa mazingira ya wachezaji wengi wa kitanzania kutegemewa na familia zao yanasababisha mshahara na posho kuwa kitu cha kwanza.
Kwa maana hiyo uongozi ukishindwa katika kipengele hiki, matatizo mengi ya uwanjani yataonekana.
Kipindi cha Rage, matatizo ya kuchelewesha posho na mishahara kwa wachezaji yameripotiwa mara nyingi na mpaka yeye mwenyeweanakiri hilo.
Uongozi kwa soka letu ndio kila kitu. Sasa safari ya Rage imefikia ukingoni na yatari uchaguzi utafanyika juni 29 mwaka huu ambapo Rais mpya , makamu wa Rais na wajumbe wapya wa kamati ya utendaji watapatikana.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa Simba sc, Damas Ndumbaro alisema jana kuwa kamati yake haitakuwa na huruma hata kidogo kwa wale wote watakaokiuka kanuni za uchaguzi.
486618_545707472135474_901587883_nNa akawaahidi wanasimba kuwa uchaguzi wa mwaka huu utazingatia misingi ya haki, kanuni na sheria kwasababu kamati yake ina watu makini, waadilifu na wenye nia ya kuisaidia Simba kupata viongozi wa kweli.
Haya ni maneno kutoka kamati ya uchaguzi, lakini bado wenye mamlaka makubwa ya kuamua nani waingie kwenye uongozi ni wanachama hai wa Simba sc.
Wanachama wa Simba mara nyingi mmetuita waandishi wa habari na kusema mengi juu ya uongozi wa Rage.
Wengi wenu hamkuupenda uongozi wa Rage na kuthubutu kusema Simba imekuwa hapa ilipo kwasababu ya mwenyekiti huyo. Sasa anaondoka na hatagombea tena.
Mambo kadhaa mnayotakiwa kuzingatia ni pamoja na kutambua kuwa klabu yenu inahitaji kiongozi mpya kwa kila kitu, zaidi awe na mawazo chanya kwa ajili ya kuiendeleza klabu.
Rais wenu awe mpenzi wa Simba, aipende Simba na atumie muda wake kuisaidia Simba sc.
Awe kiongozi mwenye mtazamo wa mbali ili katika kipindi chake cha miaka miwili ya uongozi, tuione Simba mpya.
Tunajua mna hamu ya kurudisha heshima yenu, na kwa kuanza, lazima mhakikishe juni 29 mnachagua mtu mwenye nia na sera nzuri kwa klabu ya Simba.
RAGEMwenyekiti wa Simba sc, Ismail Aden Rage anaondoka zake
Simba na Yanga zimekuwa kitega uchumi kwa watu fulani. Kuna kiongozi mmoja wa soka aliwahi kusema tukiwa katika mazungumzo ya kwaida tu kuwa hakuna hela rahisi kama kwenye mpira.
Alimaanisha kwenye mpira kuna mwanya mkubwa wa kuchuma pesa na ukajenga nyumba, ukaendesha gari na kufanya mambo mengine bila kutumia nguvu.
Simba ni klabu kubwa yenye rasilimali. Hivyo kuna watu wana nia ya kuomba uongozi ili wajinufaishe wenyewe.
Wataomba wengi , lakini watakuwa na nia tofauti. Ni ngumu sana kumjua mtu mwenye nia nzuri kwa kumuangalia machoni.
Kidogo unaweza kujiridhisha kuwa fulani hafai kama aliwahi kuwa kiongozi kwasababu unajaribu kukumbuka mazuri yake na mabaya yake, lakini kwa mtu mpya kabisa ni ngumu sana.
Kama baadhi ya watu waliowahi kuwa viongozi watarudi kwenye uchaguzi huu, basi wanachama kaeni chini mtathimini kwa kina kama wanaweza kuja na mambo mapya.
Kila kitu kipo juu yenu, mtakayemchagua ni ninyi na mtakaokuja kujuta ni ninyi. Wanachama wa Simba, kuweni makini kipindi hiki na msiridhishwe na siasa nyepesi. Mpira ni vitendo na si maneno.
Kwa bahati mbaya watanzania wengi tunaingiza siasa hasa kwenye masuala ya msingi. Ni rahisi mtu kutamka kuwa nitaijengea klabu uwanja, lakini ikifika utekelezaji, maneno ya siasa yanatumika.
Kila la heri Simba kuelekea katika uchaguzi wenu juni 29 mwaka huu, kazi imebaki kwenu kwa mujibu wa katiba ya klabu yenu.

0 comments:

Chapisha Maoni