TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wameagizwa kuchunguza na kujiridhisha kama kweli upo uchotaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow iliyokuwa imefunguliwa ndani ya Benki Kuu (BoT) kwa ajili ya kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, alisema hayo jana bungeni mjini Dodoma wakati
akihitimisha mjadala wa wabunge kuhusu bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15
ya ofisi yake ambayo jana wabunge walipitisha bajeti hiyo ya Sh trilioni
tano.
Alisema
baada ya tuhuma hizo kuanza kujitokeza, aliamua kumwuliza CAG ni namna
gani wafanye kuhusu masuala hayo. “CAG akaniambia alipoona kwenye
magazeti akaamua kuyafanyia kazi,” alisema.
Kwa
mujibu wa Pinda, CAG alizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliakim Maswi na Gavana wa Benki Kuu, Benno Ndulu, Mkurugenzi
Mtendaji wa Tanesco, Felschemi Mramba ili kupata picha ya yaliyojiri
katika mchakato mzima.
Alisema
Katibu Mkuu, Nishati na Madini pia alimwandikia barua kumwomba CAG
afanye uchunguzi wa kina ili tuhuma hizo zilizotolewa kwenye vyombo vya
habari, zipatiwe ufumbuzi.
“Maelezo
niliyoyapata, kamati ya PAC ilipokuwa imemwita Katibu Mkuu kuhusu jambo
hilo, alitoa maelezo kwamba ameshamwelekeza CAG kufanya uchunguzi
kuhusu jambo hilo. PAC nayo ilimwandikia CAG afanye uchunguzi.
“Na
mimi nimemwambia CAG fanya uchunguzi wako halafu tuletee serikalini
tuletee bungeni…kwa tuhuma zenyewe zilivyo, itabidi tuwahusishe na
Takukuru nao ili nao watusaidie kupata ukweli juu ya jambo hili. Kwa
sababu kwa maelezo na mtiririko ulivyo ni tuhuma zinazojitokeza ambavyo
vyombo hivi vinao uwezo kubaini kipi cha ukweli na kipi si cha kweli,”
alisema na kuomba Bunge likubali CAG akamilishe kazi hiyo.
Pinda
alisema uamuzi wa kuingiza takribani Sh bilioni 20 katika akaunti ya
Escrow haukuwa wa kificho kwa kuwa fedha hizo zilikuwa za IPTL na ndivyo
mahakama ilivyokuwa imeelekeza. Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, suala la
IPTL ni la muda mrefu tangu 1994.
Wakati huo serikali baada ya kuona lipo tatizo la umeme, ilitafuta mtu aliyekuwa tayari kuzalisha umeme.
Mkataba
ulionesha umeme utakaozalishwa utauzwa Tanesco na ulikuwa na sehemu
mbili kwa maana ya malipo ya uwepo wa mtambo na pia uzalishaji.
Wakati
wakiendelea, ulitokea mgogoro upande wa Tanesco na IPTL kuhusu kodi
inayopaswa kulipwa na baadaye ukazaa kesi iliyobidi ipelekwe mahakama ya
kimataifa ya usuluhishi.
Wakati
mgogoro huo ukiendelea, Serikali ilibidi ifungue akaunti ya Escrow na
fedha kutoka Tanesco zikawa zikilipwa kwenye akaunti hiyo. Fedha
zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti hiyo ni za IPTL na katika uamuzi wa
mahakama ikaamriwa fedha hizo zipelekwe IPTL kwa kuwa ni fedha zao.
Kukawa na mvutano.
“Fedha hizo zikapelekwa IPTL, jambo tunalopaswa kama wabunge kujiridhisha nalo ni je, VAT ipo kweli au haipo?,” alisema Pinda.
Alisema
baada ya kesi kumalizika, Tanesco na IPTL walikaa wakatazama kiasi
kinachodaiwa, wakafika mahali wakakubaliana ni kiasi gani cha fedha
kilipwe. Alisema kwa upande huo, kama kuna masuala yanaweza kupatiwa
majibu bila mjadala na kuvutana.
“Kubwa
ni pale zogo limejikita zaidi kwenye kuondoa fedha kutoka akaunti ya
Escrow kutoka Benki Kuu kupeleka IPTL na maswali ambayo yamejitokeza
kwamba kodi haikulipwa, ufisadi upo, unajiuliza wa nini kama fedha ile
ilikuwa ni fedha yao,” alihoji Pinda.
Ufafanuzi
huo wa Waziri Mkuu ulitokana na kauli iliyotolewa juzi na Mbunge wa
Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi) akituhumu baadhi ya
viongozi na watendaji serikali kuchota fedha hizo katika akaunti hiyo.
Mbunge
huyo alitawataja Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, Katibu
Mkuu wa wizara hiyo, Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick
Werema kwamba walihusika.
Mpina
amsuta Kafulila Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luhaga Mpina amepinga kauli iliyotolewa
na Kafulila bungeni juzi akisema Gavana wa BoT aliiambia kamati hiyo
kuwa alilazimika kuruhusu fedha zitolewe kutokana na shinikizo la vigogo
wa serikali. Mpina ambaye aliomba mwongozo wa spika jana, alikanusha
Gavana huyo wa Benki Kuu kuiambia kamati yake maneno hayo.
“Nilidhani
mimi ndiye sikusikia maneno hayo; lakini nilipowasiliana na wenzangu
kwenye kamati, walisema suala hilo halikusemwa,” alisema Mpina.
Aliendelea
kusema, “Watu wengine wanaweza kusema kwa sababu mimi ni mwana CCM kwa
hiyo ninapendelea, lakini kuna wabunge watano kwenye kamati kutoka
upinzani waliosema Gavana wa BoT hakusema hivyo.” Mpina alisema kamati
yake ilimwandikia gavana wa benki kuu kufika kwenye kamati yao kuhusu
suala hilo la fedha za akaunti ya Escrow.
Alisema,
“Baada ya Kafulila kuzungumza hilo, niliwaita wajumbe wangu,
tukaulizana, kila mmoja alisema si kweli kilichosemwa. Kila kitu ninacho
hapa tena kwa maandishi, nitawasilisha kwako mheshimiwa Spika.”
AG
azungumza Wakati baadhi ya wabunge jana walishinikiza Waziri Mkuu aunde
tume ya bunge kuchunguza suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG),
Jaji Werema alisema fedha hizo haziko mikononi mwake.
“Mnapomuuliza
Waziri Mkuu akubali kuundwa kwa kamati, kwa mujibu wa kanuni hiyo siyo
kazi yake. Huo ni wajibu wa spika ndivyo inavyosemekana. Lakini wazo na
hapa lazima kama kuna mafisadi, na Werema anatajwa ni miongoni, lazima
ijulikane. Wala hakuna kufunika vitu vyote viko wazi na mimi ninavyo vya
wazi vingi kabisa…na uamuzi uliofanyika, uchunguzi ufanywe na CAG ni
sawa sawa,” alisema.
Spika
aonya wabunge kutumiwa Wakati huo huo Spika wa Bunge, Anne Makinda,
ameonya wabunge dhidi ya kutumiwa na watu wengine wa nje ya Bunge kwa
manufaa yao.
Makinda
alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wakija bungeni wakiwa wamebeba hoja
za watu binafsi na kuzitetea. Katika kile alichosema vitendo hivyo
vinaweza kuhatarisha uhai wa bunge, alisema hata kama mbunge ameambiwa
jambo nje ya Bunge, ni lazima kulipima kabla ya kulileta bungeni.
“Sasa
nimeanza kuona kuna baadhi yetu wanakuja na hoja zao kutoka nje na
kuzileta humu kuzitetea,” alisema na kusisitiza kuwa kitendo hicho si
sahihi na kinaharibu heshima ya bunge.
Ingawa
alisema ushawishi ni suala la kawaida, lakini alisema mbunge anapopata
mawazo ya mtu mwingine, anapaswa kuchanganya na ya kwake na si kuingiza
hoja hiyo moja kwa moja bungeni.
0 comments:
Chapisha Maoni